JAYRUTTY Yashinda Zabuni Jezi za Simba, Kununua basi jipya na Kujenga Uwanja

JAYRUTTY Yashinda Zabuni Jezi za Simba, Kununua basi jipya na Kujenga Uwanja
JAYRUTTY Yashinda Zabuni Jezi za Simba, Kununua basi jipya na Kujenga Uwanja
Klabu ya Simba imeitangaza Kampuni ya Jayrutty Investment Limited kushinda tenda ya usambazaji wa jezi za klabu ya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano (5).
Mwenyekiti wa Kamati ya Tenda Dkt. Seif Muba amesema kuwa kampuni hiyo imeweka kiasi cha fedha Tsh. 38 Bilioni ambapo klabu ya Simba inakwenda kupata Tsh. 5.6 Bilioni kwa kila mwaka.

Dkt. Seif Muba Mwenyekiti wa Kamati ya Tenda Simba Sc
Aidha katika kipindi cha miaka mitano, kampuni hiyo itaboresha miundo mbinu ikiwa ni pamoja na kununua basi jipya, kujenga uwanja utakaochukua kati ya mashabiki 10,000-12,000, kujenga ofisi rasmi za klabu na studio kwaajili ya kitengo cha habari na Mawasiliano.
“Tulipokea barua nyingi za maombi lakini bodi iliamua makampuni yashindane kwa tenda. Kampuni nane zilichukua tender document lakini kampuni sita zilirudisha document. Maombi ya wazabuni yalifunguliwa kwa uwazi na baada ya mchakato wazabuni wote walijulishwa mzabuni ambaye ameibuka mshindi kwa kuweka fedha na vitu vingi ambavyo tulihitaji. Tuliingia mkataba wa miaka mitano na kampuni hiyo”
“Mshindi aliyeshinda tenda hiyo ameshinda kwa kuweka kiasi cha fedha cha Tsh. 38 Bilioni. Napenda kuitangaza kampuni ya Jayrutty Investment Company Limited kama mshindi. Klabu ya Simba inakwenda kupata Tsh. 5.6 Bilioni kwa mwaka,” alisema Muba
Naye Mkurugenzi wa Jayrutty Investment Company Limited, CPA Joseph Rwegasira amesema kuwa tayari kampuni hiyo imetoa asilimia 30% ya kiasi cha fedha ambazo wanapaswa kutoa katika mwaka wa kwanza wa tenda hiyo
“Kiasi ambacho kimetajwa ni kiasi ambacho tumezingatia mambo mengi kama klabu. Nipende kuwahakikishia kabla hata hatujafanya kitu chochote tumeshaweka 30% ya hiki kiasi cha mwaka wa kwanza.”

CPA Joseph Rwegasira Mkurugenzi wa Jayrutty Investment Company Limited
“Jambo la kwanza ambalo tunakwenda kutekeleza ni kujenga uwanja wa mpira, uwanja ambao utachukua mashabiki 10,000 hadi 12,000 na tumekubaliana kwamba Simba wana uwanja Bunju na tutakwenda kujenga uwanja Bunju lakini kama watakuja na mapendekezo mengine basi tutayafata”
“Simba ni timu kubwa Afrika na sisi tumesema kwamba tutanunua basi jipya la Irizar, kila kitu kipo sawa. Muda si mrefu mtaliona hapa. Tutaangalia pia upande wa media, tunakwenda kujenga media kubwa kama klabu zingine kubwa na tumeshaanza utaratibu.”
“Tunajua kwamba Simba makao makuu yapo Msimbazi lakini tunakwenda kujenga ofisi za kisasa. Lakini pia kila mwaka tutatoa Tsh. 100 milioni ya kusaidia kukuza soka la vijana. Kila mwaka pia tutachangia Tsh. 100 milioni kuchangilia pre season. Pia tumeahidi kujenga kituo maalumu cha matibabu ya wachezaji. Kila mwaka pia tutashiriki bega bega katika Simba Day, tutachangia Tsh. 100 milioni kila mwaka.”
“Hizi ni baadhi ya faida za ziada ambazo sisi tutatoa kwa Simba Sports Club. Kila mwaka tumekubali kutoa Tsh. 470 milioni kwa wachezaji, uongozi utagawa kwa namna ambayo wataona inafaa na hii fedha itakuwa inaongezeka kila mwaka.”
“Tumeenda kimataifa kuhakikisha tunapata international brand, niwahakikishie kwamba msimu unaokuja jezi ambayo Simba watavaa, watavaa jezi ya kimataifa. Tumeingia mkataba wa kimataifa na brand mojawapo kubwa duniani ambayo inazivisha klabu nyingi kubwa,” alisema Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Jayrutty Investment Company Limited, CPA Joseph Rwegasira
“Kila mwaka tutasajili mchezaji mmoja ambaye Wanasimba wanamtaka, tutakuwa tunaambiwa na sisi tutakuwa tunamsajili.”- Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Jayrutty Investment Company Limited, CPA Joseph Rwegasira
“Kamati ya tenda iliundwa na wenyeviti wa kamati ndogo za bodi. Mimi nawapongeza sana wajumbe hawa kwa kazi kubwa waliyofanya kwa niaba ya bodi. Bodi nzima iliridhia kwamba hakuna sababu aliyeshinda kutokupewa hii tenda.”

Murtaza Mangungu Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC
“Mapinduzi makubwa ya jezi yalifanywa na Kassim Dewji kwa zaidi ya miaka 10. Miaka hiyo tulikuwa tunaletewa tu jezi nyeupe na nyekundu lakini yeye akaleta jambo la tofauti lakini game changer ni Vunja Bei yeye ndio akuja kuonyesha njia, Sandaland alifanya kazi yake lakini sasa amekuja Jayrutty.”
“Umeahidi mambo mengi uyafanyie kazi usijesema kwamba ulitamani brand kubwa lakini imeshindakana. Nawahakikishia Wanasimba wote tutashirikiana kufanikisha hilo. Tutashirikiana na mpango wa mwekezaji Mohammed Dewji hivyo hakutakuwa na kuingiliana katika utekelezaji wake.”- Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu.
“Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu imewekeza sana kwenye michezo na hasa mchezo huu pendwa wa mpira wa miguu. Ki takwimu hakuna kipindi tumefanya vizuri kama kipindi hiki. Mchezo huu unaendelea kutupa raha mioyoni na kututangaza nje ya mipaka ya nchi.”

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma
“Hili nililosikia leo la ujenzi wa uwanja limenivutia sana. Mkiwa na kiwanja cha watu 10,000 au 12,000 kinaweza kutumika kwa michezo ya ndani, michezo ya nje ndio mkawa mnatumia Uwanja wa Mkapa, mtaupunguzia hata majukumu.”
“Itoshe kusema ni uwekezaji wa mkakati ambao umekuja wakati sahihi. Serikali kama mlezi wetu tunawapongeza sana.”
“Naamini mna maarifa ya kucheza mchezo wa nusu fainali utakaochezwa Zanzibar na kule Afrika Kusini na kuhakikisha mnavuka na kuingia fainali hadi kushinda ubingwa wa Afrika. Na sisi kama serikali kama mara zote ambavyo tunawaunga mkono hatutawaacha hata wakati huu. Tupo nyuma yenu kuhakikisha mnashinda ubingwa wa Afrika. Hatuishii Hapa.”- Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma.
Je, Unatafuta Nafasi za kazi?Jiunge na Watanzania wengine Kupata Matangazo ya Ajira Kila Siku Kutoka Serikalini pamoja na Makampuni Mbalimbali.
Kupata Matangazo ya Ajira Kila Siku ni bure kabisa, JIUNGE HAPA
JIUNGE NA GROUP LETU HAPA, JIUNGE NA CHANNEL YETU HAPA, JIUNGE NA TELEGRAM HAPA.

Tags: JAYRUTTY Yashinda Zabuni Jezi za Simba, Kununua basi jipya na Kujenga Uwanja