MAGAZETI ya Tanzania Leo Jumapili 09 February 2025
MAGAZETI ya Tanzania Leo Jumapili 09 February 2025
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) bado inakabiliwa na mwendelezo wa migogoro ambayo athari zake zinavuka mipaka na kusababisha madhara kwa nchi jirani.
Amebainisha hayo alipokuwa akizungumza wakati akiwakaribisha wageni kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Jumamosi February 8, 2025 Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Kama viongozi wa kanda, historia itatuhukumu kama tutakaa tukitazama hali ikizidi kuwa mbaya kila siku. Nchi zetu zina wajibu wa pamoja kuhakikisha tunatatua changamoto ya usalama iliyopo ambayo imeathiri ustawi wa raia wasio na hatia,” amesema Rais Samia.
Amesema mgogoro unaoendelea si tu unaiathiri DRC, lakini pia, unahatarisha juhudi za mara kwa mara za kuleta utengamano wa kikanda.
“Tunatakiwa kuamini kwamba, mkutano huu utakuja na mapendekezo na hatua za kutatua mzozo unaoendelea DRC ili kulinda haki za binadamu,” amesema Rais Samia kwenye mkutano huo wa dharura unaolenga kutatua mzozo mashariki mwa DRC.
Naye Rais wa Kenya, William Ruto ambaye pia ni Mwenyekiti wa EAC amesema kuwa eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) limekuwa katika vita kwa miongo miwili na kugharimu maisha ya maelfu ya watu wakikimbia makazi yao.
Akizungumza wakati wa hotuba yake ya ufunguzi February 8, 2025 katika mkutano wa viongozi wa mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), amesema wamekutana pamoja kutoa kauli kwa pande zinazohusika katika mgogoro huo, kusitisha uhasama baina yao.
“Tunasimama pamoja kuzitaka pande zote kusitisha mapigano mara moja hususani M23 kuacha kusonga mbele na vikosi vya DRC kusitisha operesheni zao za kijeshi dhidi ya M23.
“Kusitisha mapigano mara moja ndiyo njia pekee, tunaweza kutengeneza masharti muhimu ya majadiliano ya kujenga na utekelezaji wa makubaliano ya amani,” amesema Ruto.
Kwa upande wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kupitia ukurasa wake wa X, ameandika kuwa, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi anapaswa kuzungumza moja kwa moja na watu anaozozana nao.
Rais Museveni ametoa pendekezo hilo wakati mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaendelea jijini Dar es Salaam.
“Leo nimehudhuria mkutano wa EAC, SADC, Dar es Salaam, Tanzania unaolenga hali inayoendelea DRC mapendekezo yangu ya awali katika mkutano huu ni Rais Tshisekedi azungumze moja kwa moja na watu wenye ugomvi naye kwa sababu hii inatuathiri sote.
“Hakuna jukwaa lingine bora zaidi la kujadili suala hili kuliko mkutano huu. Hivyo, ninatarajia mjadala mzuri na wenye matokeo chanya, “ameandika Rais Museveni kupitia ukurasa wake wa X.
Viongozi hao wanaendelea na mkutano leo Jumamosi Februari 8, 2025 Ikulu jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta suluhu ya mapigano yanayoendelea mashariki mwa DRC baina ya majeshi ya Serikali dhidi ya vikosi vya M23.
TAZAMA AJIRA ZOTE TANZANIA
Je, Unatafuta Nafasi za kazi?Jiunge na Watanzania wengine Kupata Matangazo ya Ajira Kila Siku Kutoka Serikalini pamoja na Makampuni Mbalimbali.
Kupata Matangazo ya Ajira Kila Siku ni bure kabisa, JIUNGE HAPA
