Taarifa Muhimu Kuhusu Mchakato wa Ajira za Ualimu

Taarifa Muhimu Kuhusu Mchakato wa Ajira za Ualimu
Taarifa Muhimu Kuhusu Mchakato wa Ajira za Ualimu
Kutokana na upotoshaji unaoendelea kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii kuhusu mchakato wa ajira za walimu unaoendelea katika Mikoa yote nchini, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeona upo umuhimu wa kutoa ufafanuzi juu ya suala hili.
Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilianzishwa kama sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, kifungu cha(4.2)(ii)(iii) inayoelekeza kuwa: Ajira za ushindani zifanyike katika madaraja ya kuingilia kwenye miundo ya utumishi; na Kiundwe chombo cha ajira katika Utumishi wa Umma kitakachokuwa kinashughulikia na kusimamia upatikanaji wa wataalamu mbalimbali.
Katika kuwezesha utekelezaji wa Sera hii, Kifungu cha 29 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, kinaelekeza kuwepo kwa chombo maalumu cha kushughulikia mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma. Kanuni za Uendeshaji wa Shughuli za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2021 zilizotolewa.
kupitia Tangazo la Serikali Na.580 la Mwaka 2022 ndizo zinazozingatiwa katika utekelezaji wa majukumu yake.
Vilevile, Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023, kifungu cha (3.12.1.5) inaelekeza kuwa: Serikali itaimarisha mfumo wa ajira ya walimu, wakufunzi, na wahadhiri kwa kuhakikisha kuwa wenye sifa na viwango stahiki wanaajiriwa baada ya kufanya mitihani na kufaulu kama sehemu ya usaili.
LENGO LA KUANZISHWA KWA SEKRETARIETI YA AJIRA
Lengo kuu la kuundwa kwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni kuziwezesha Mamlaka za Ajira kupata nafasi ya kutekeleza majukumu yao ya msingi kama yalivyoainishwa katika miongozo ya uanzishwaji wa Taasisi hizo (Instruments).
MCHAKATO WA AJIRA UNAVYORATIBIWA
Mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma huendeshwa na Sekretarieti ya Ajira kwa niaba ya mamlaka za ajira katika Utumishi wa Umma zinazojumuisha: Wizara, Idara Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa, Wakala za Serikali; Mamlaka za Serikali za Mitaa; Taasisi na Mashirika ya Umma.
Sheria iliyoanzisha Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeweka bayana mipaka ya majukumu ambapo, ajira zote zinazohusu: Mhimili wa Bunge; Mhimili wa Mahakama; na vyombo vya ulinzi na usalama zinaendelea kusimamiwa na mihimili na taasisi hizo na hivyo kutoihusisha Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Vile vile, Kifungu cha 29(A) (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma ili kukidhi mahitaji ya Serikali, kimempa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira uwezo wa kukasimu madaraka kwa Afisa Mtendaji Mkuu au kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuendesha mchakato wa ajira. Pia, Sheria inampa uwezo Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuchukua majukumu aliyoyakasimu kwa taasisi nyingine kadiri atakavyoona inafaa.
Kwa sasa, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma amezikasimu madaraka ya kuratibu mchakato wa ajira taasisi mbalimbali za Umma ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BOT); Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kada 23; pamoja na vyuo Vikuu vya Umma kwa kada za wanataaluma. Taasisi hizi zinapoendesha mchakato wa usaili huishirikisha kwa karibu Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ili kuhakikisha taratibu zinazohusu mchakato wa ajira zinafuatwa ipasavyo.
UTARATIBU WA KUTOA MATANGAZO YA AJIRA.
Baada ya kupokea vibali vya ajira na kuvichambua kwa kushirikiana na waajiri, Sekretarieti ya Ajira huandaa na kutoa matangazo ya nafasi za kazi kupitia tovuti yake (www.ajira.go.tz). Pia, hutumia akaunti rasmi za mitandao ya kijamii ya ‘Facebook’, ‘Twitter’ (X), Instagram na Whatsapp channel.
Sekretarieti ya Ajira kupitia TEHAMA, pia imeunda Mfumo wa Programu ya Rununu “Ajira Portal Mobile App” kwa watumiaji wa vifaa vya ‘Android’ na ‘iOS’ ambao humpa taarifa mwombaji kazi juu ya uwepo wa nafasi za ajira. Vilevile, waombaji waliojisajili kwenye Mfumo wa Kidigitali wa USSD; hupokea taarifa za uwepo wa ajira kupitia simu zao za kiganjani. Hata hivyo, ili mwombaji wa ajira aweze kupokea taarifa za ajira, anatakiwa ajisajili, kwa kubofya *152*00# na kisha kufuata maelekezo.
Matumizi ya mifumo ya TEHAMA yameboresha utoaji huduma pamoja na kupunguza gharama kwa Serikali na waombaji wa fursa za ajira tofauti na mfumo uliotumika awali wa njia ya magazeti, redio na runinga katika kutoa matangazo na kuita waombaji kwenye usaili. Matangazo hayo pia yalikuwa hayawafikii wadau wote kwa wakati.
UTARATIBU WA KUPOKEA MAOMBI YA KAZI
Maombi ya kazi kutoka kwa waombaji wa fursa za ajira hupokelewa kwa njia ya TEHAMA kwa kutumia Mfumo wa Kidigitali wa Ajira Portal’ ambao humuwezesha mwombaji kutuma maombi yake ya ajira popote alipo kwa njia ya kidigitali (Online Application). Mfumo huu humpa mrejesho wa papo kwa papo endapo maombi yake yamepokelewa ama la. Tofauti na zamani maombi yalipokuwa yanapokelewa kwa njia ya posta.
UTARATIBU WA KUCHAKATA MAOMBI YA AJIRA
Uchakataji wa taarifa za waombaji fursa za ajira wanaowasilisha maombi ya ajira hufanyika kwa njia ya kidigitali mara tu baada ya tangazo la kazi linapoisha muda wake. Baada ya hatua hiyo, maafisa wa Sekretarieti ya Ajira huoanisha taarifa zilizowasilishwa na waombaji na sifa zilizoainishwa kwenye tangazo la kazi ili kupata orodha fupi ya waliokidhi vigezo na wanaopendekezwa kuitwa kwenye usaili kwa hatua zaidi.
UTARATIBU WA USAILI
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inaendesha usaili kupitia njia tatu (3). Na hii ni kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji wa Shughuli za Sekretarieti ya Ajira za Mwaka 2021. Utaratibu huu huzingatia mahitaji ya kada na nafasi inayotakiwa kujazwa kama ifuatavyo:
USAILI WA KUANDIKA (APTITUDE TEST)
Huu ni usaili wa kuandika ambao hufanyika ili kufanya mchujo na kupata waombaji wote wenye sifa pale ambapo idadi ya waombaji ni kubwa kuliko fursa zilizopo. Utaratibu huu hutoa fursa kwa waombaji wote wenye sifa kushindania nafasi katika hatua inayofuata.
USAILI WA VITENDO (PRACTICAL)
Usaili wa vitendo hufanyika kwa baadhi ya kada kama vile Udereva; Katibu Mahsusi; wataalam wa TEHAMA; na kada nyingine zenye mahitaji kama hayo. Lengo ni kupima uwezo na ujuzi wa utendaji kazi katika fani husika.
USAILI WA MAHOJIANO YA ANA KWA ANA (ORAL INTERVIEW)
Usaili wa mahojiano huwa ni hatua ya mwisho ya kuwachuja wasailiwa ili kupata wanaofaa kuajiriwa katika utumishi wa Umma.
KUKASIMISHA MAMLAKA YA KUAJIRI KWA BAADHI YA WIZARA NA TAASISI
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilipoanza utekelezaji wa majukumu yake Mwaka 2010, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma alikasimu majukumu ya kuajiri watumishi wa kada za afya, ualimu, mifugo, kilimo na uhasibu kwa Wizara za kisekta. Uamuzi huu ulitokana na uhaba wa wataalamu wa kada hizo katika soko la ajira kwa wakati huo na hivyo kutokuwepo sababu za kuwashindanisha. Hata hivyo, kutokana na ongezeko la wataalamu wa kada hizo katika soko la ajira kwa sasa, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa miaka tofauti baada ya kushauriana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inayosimamia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma na mamlaka nyingine za ajira, imekuwa ikirejesha kwake mamlaka ya kuajiri yaliyokuwa yamekasimishwa kwa Wizara na Taasisi hizo ili kuruhusu ushindani kama ilivyo kwa wataalamu wa kada nyingine.
USAILI WA KADA ZA UALIMU
Usaili wa kada za ualimu kujaza nafasi 14,648 zilizotolewa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu nchini ulianza tarehe 14 Januari, 2025 na unatarajiwa kukamilika tarehe 24 Februari, 2025 Tanzania Bara na Zanzibar. Hadi tarehe 18 Februari, 2025, jumla ya walimu 6,055 waliofanya usaili na kufaulu wamepangiwa vituo vya kazi katika maeneo mbalimbali nchini baada ya kukamilika kwa mchakato wa ajira zao.
Ili kutekeleza dhana ya uwazi, usaili wa kada za ualimu unasimamiwa kwa ushirikiano wa viongozi kutoka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma; Ofisi ya Rais (UTUMISHI); Ofisi ya Rais (TAMISEMI); Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Tume ya Utumishi wa Walimu; Taasisi nyingine za Umma; pamoja na Ofisi za Wakuu wa Mikoa kote nchini. Aidha, wataalam wanaohusika na usahihishaji wa mitihani ya usaili pamoja na wale wanaoshiriki kwenye majopo ya usaili wameratibiwa na Katibu wa Sekretareti ya Ajira kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa chini ya uratibu wa Makatibu Tawala wa Mikoa.
Matokeo ya usaili wa kada za ualimu yamekuwa yakiingizwa kwenye mfumo wa kidigitali wa ‘Ajira Portal’ mara baada ya usaili kukamilika kwenye vituo husika katika Mikoa yote nchini. Jukumu hili husimamiwa na timu za viongozi kutoka Makao Makuu-Dodoma na Ofisi za Wakuu wa Mikoa. Wasailiwa waliofanya vizuri katika usaili huu wamepata fursa ya kuajiriwa na waliofaulu na kukosa nafasi katika usaili majina yao yataendelea kuhifadhiwa katika Kanzidata ya Sekretarieti ya Ajira kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa msingi huu, Serikali ikitoa vibali vya ajira au nafasi za ajira zikipatikana kutokana na sababu mbalimbali watapangiwa vituo vya kazi bila kulazimika kurudia kufanya usaili.
Hivyo, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inapenda kuwakumbusha wale wote wanaotoa taarifa za kupotosha kuhusu mchakato wa ajira za walimu unaoendelea nchini kote kuacha upotoshaji huo. Vilevile, tunawaomba wadau wote kupuuza upotoshaji huo kwani lengo la utaratibu huu ni kupata nguvu kazi ya walimu wenye uwezo na weledi watakaochangia katika kuifikisha nchi yetu katika malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050. Pia ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008, Toleo la 2 na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023.
Mwisho, tunawasihi wote wanaotafuta fursa za ajira katika Utumishi wa Umma wenye sifa stahiki wakiwemo walimu, kujiandaa vizuri kabla ya usaili, kujiamini na kushiriki katika usaili ili waweze kufaulu na kupangiwa vituo vya kazi kadiri nafasi za ajira zinapojitokeza.
Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inawahakikishia waombaji fursa za ajira kuwa mchakato wa ajira chini ya ofisi hii unaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi bila ya rushwa wala upendeleo wowote. Vilevile, kama wadau wetu muhimu tunawaomba mtupatie taarifa kila mtakapobaini upungufu wowote vikiwemo vitendo visivyo vya kimaadili ili sisi wenyewe kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali tuweze kuchukua hatua stahiki kwa wakati pamoja na kuboresha zaidi huduma zetu.
Je, Unatafuta Nafasi za kazi?Jiunge na Watanzania wengine Kupata Matangazo ya Ajira Kila Siku Kutoka Serikalini pamoja na Makampuni Mbalimbali.
Kupata Matangazo ya Ajira Kila Siku ni bure kabisa, JIUNGE HAPA
JIUNGE NA GROUP LETU HAPA, JIUNGE NA CHANNEL YETU HAPA, JIUNGE NA TELEGRAM HAPA.
